Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amesema kuwa bei ya Pamba itabaki kuwa Shilingi 1,200 hata kama imeshuka kwenye Soko la dunia. Amesema hayo mapema leo alipokuwa akiongea na Wakulima wa Pamba Wilayani Kahama kwenye vituo vya kuuzia Pamba.
"Wadau walikutana wakapanga bei na iliafikiwa kuwa mwaka huu bei ni 1200 kwa kilo ya Pamba.
Lakini baada ya msimu kuanza soko la dunia likashuka. Baada ya kukokotoa ikaonekana inabidi Pamba iuzwe kwa shilingi 900 kwa kilo, hali hii ikawashtua wanunuzi wakaona bei haina faida tena kwa upande wao. Lkn Serikali ikasema hapana lazima wanunuzi wanunue kwa 1200 na hiyo hasara itafidiwa na Serikali. Serikali itawalipa wanunuzi 300 ili Mnunuzi aendelee kumlipa mkulima shilingi 1200 badala ya 900". Amesema Mhe. Hasunga
Aidha Mhe. Hasunga amesema kuwa Serikali imeshafanya mkakati wa kushirikisha Benki kuu ili Mabenki yawashushie riba wafanyabiashara wenye nia ya kununua pamba. Na ameagiza kuwa ifikapo tarehe 31 Julai mwaka huu pamba yote iwe imenunuliwa na wakulima wote wawe wamelipwa hela zao.
Katika hatua nyingine Mhe. Hasunga ameagiza kuwa kuanzia mwakani hakuna mkulima atakayekopeshwa pembejeo hivyo wakulima wakiuza Pamba yao watenge hela ya kununulia pembejeo ikiwemo dawa na mbolea. Amesema hii itasaidia kuwafanya wakulima wanunue dawa wanazoziamini wao badala ya kulazimishwa dawa ambazo nyingi zinakuwa hazina ufanisi.
Mhe. Hasunga yupo kwenye ziara ya kikazi Wilayani hapa kwa siku moja na ametembelea vituo vya kuuzia Pamba na kuongea na wakulima kila kituo.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa