Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria wote walioshiriki kuuza eneo la Chuo cha Ufundi "MWAMVA" kilichopo Mjini Kahama baada ya agizo la Mhe. Rais la kutaka ekari arobaini za chuo zilindwe.
Amesema haya mapema jana alipotembelea eneo hilo na kuongea na wananchi waliovamia eneo la chuo ikiwa ni sehemu ya ahadi aliyoitoa mwezi mmoja nyuma kuwa atatembelea hapo.
Telack amesema kuwa kitendo cha kuendelea kuvamia na kuuza eneo lililotengwa kwa ajili ya Chuo ni kupingana na Rais.
"Siku zote huwa nasema kuwa suala likishazungumzwa kwamba ni la serikali tunatakiwa tuelewe na tutii, hakuna asiyejua kuwa eneo hili ni la Chuo... Serikali ikiamua imeamua na tayari Mheshimiwa Rais amekwisha sema kuwa eka arobaini ni za Chuo na sisi hapa tunasimamia eka arobaini. Kwahiyo kama kuna mtu yupo ndani ya mipaka ya hizi eka arobaini ajue yupo kwenye eneo ambalo sio la kwake na anatakiwa kutoka." Amesema Telack.
Katika hatua nyingine Mhe. Telack ameagiza kuwa wale wote waliohusika kuwadanganya na kuwauzia wananchi eneo la Chuo wachukuliwe hatua kwani ndio chanzo cha migogoro.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa