Halmashauri ya Mji wa Kahama imezindua maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani kwa kufanya maonesho ya Mifuko mbadala na kukaribisha wadau kuchangamkia fursa za mifuko hiyo.
Uzinduzi huo umefanyika mapema leo kwenye viwanja vya National Housing karibu na lililokuwa soko la Wakulima.
Leo ni siku ya kwanza kati ya siku tano kuelekea siku ya mazingira Duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo Juni 5 kila mwaka.
Katika siku tano hizi wataalamu watakuwepo eneo hilo kwa ajili ya kutoa uelewa wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali juu ya Mazingira.
Aidha kutakuwa na maonesho ya mifuko mbadala na maelezo ya kina juu ya ambao bado wana mifuko ya plastiki.
Akiongea katika uzinduzi huo Afisa Mazingira wa Mji wa Kahama Ndg. Johannes Mwebesa amesema kuwa hadi sasa hivi zaidi ya Kilo themanini za mifuko ya plastiki imekusanywa kupitia maeneo yaliyobainishwa ambayo ni ofisi za Kata na Makao makuu ya Halmashauri ya Mji wa Kahama.
"Bado zoezi linaendelea la kupokea mifuko na kutoa elimu hivyo nawaomba wana Kahama wote ambao bado wana mifuko ya plastiki waweze kuiwasilisha kwenye maeneo hayo" Amesema Ndg. Mwebesa
Afisa huyo amebainisha kuwa mifuko ya plastiki ambayo inaendelea kukusanywa inatunzwa na kusubiri maelekezo kutoka ofisi za Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambao watatoa mwongozo na utaratibu ulio bora wa kuiteketeza.
Bwana Mwebesa amewataka wana kahama kujitokeza kwa wingi katika siku hizi tano ili wapate kujua yale ambayo walikuwa hawayajui.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa