Kampuni ya uchimbaji madini ya Twiga Minerals Corporation kupitia mgodi wake wa dhahabu wa Barrick Buzwagi imekabidhi hundi yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.15 (1,159,817,107.83/=) kwa halmashauri ya Mji wa Kahama ikiwa ni malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2020.
Akikabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama, Mhe. Anamringi Macha leo Jumatano Julai 15,2020,Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi, Benedict Busunzu amesema lengo la mgodi huo ni kuona mamlaka husika zinaelekeza fedha hizo katika miradi inayolenga kuwaletea maendeleo wananchi wanaozunguka migodi.
“Migodi ya Twiga Minerals chini ya Kampuni ya Barrick nchini Tanzania hulipa ushuru wa huduma kila baada ya miezi sita kwa halmashauri ili ambazo migodi yetu inaendesha shughuli zake kulingana na mapato ya kila mwaka ambapo malipo haya ni kutekeleza hitaji la kisheria na ni sehemu ya mikataba ya makubaliano kati ya migodi na halmashauri husika”,aliongeza Busunzu.
“Tunatoa ushuru ili kuboresha utoaji wa huduma katika jamii zinazozunguka migodi katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu,afya na upatikanaji wa maji safi na salama”,alisema.
Aidha alisema licha ya mgodi huo kulipa kodi stahiki bado imekuwa ikijishughulisha katika kuhakikisha inakuwa mdau muhimu wa maendeleo kupitia sera yake ya maendeleo ya jamii ikiwa ni kuunda fursa endelevu za kiuchumi na maendeleo katika jamii na kuinua uchumi wa wilaya na kuboresha ustawi wa maisha ya wenyeji.
Akipokea hundi hiyo, Mkuu wa wilaya ya Kahama,Mhe. Anamringi Macha aliipongeza kampuni ya Twiga Minerals kwa kutoa ushuru wa huduma ikiwa ni zao la kwanza chini ya Twiga iliyotokana na ubia kati ya serikali na Barrick huku akiiagiza halmashauri kutumia fedha hizo kwa utaratibu utakaoleta tija kwa wananchi.
“Sisi tunataka fedha zinaenda kwenye miradi ambayo itakuwa na tija kwa ajili ya maendeleo ya vijana, watu wenye ulemavu,wanawake. Mkono wa serikali bado upo pale pale kuhakikisha fedha hizi zinakwenda kutekeleza ile miradi tuliyoikusudia”,alisema Macha.
Alisema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo katika jamii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika sekta ya elimu,afya,maji na miradi mingine itakayogusa wananchi moja kwa moja.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa