Timu ya Wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Kahama (CMT) ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mji Ndg. Anderson Msumba imeamua kuendesha baadhi ya Vikao vyake vya Mwezi kwenye maeneo ya Shule ambako kuna changamoto mbalimbali ili wajionee wenyewe na hatimaye wafanye maamuzi yenye matokeo chanya na yanayoakisi uhalisia. Kikao cha kwanza kimefanyika mapema leo kwenye Shule ya Msingi Ntungulu iliyopo kata ya Kilago ambako moja kati ya maazimio ya Kikao hicho ni kuhakikisha wanapatiwa huduma ya maji japo ya visima vifupi na nyumba zote za Watumishi zinazojengwa ambazo zipo pembezoni mwa mji lazima ziwekewe Umeme wa Jua, seti za runinga ikiwemo Dishi na King'amuzi ili kuwafanya watumishi hao kujisikia wapo sawa na wale wanaoishi Mijini na kuwajengea morali ya kufanya kazi.
"Kwanza niseme tumefarijika sana kwa ukarimu wenu, lakini lengo kubwa la kuja huku ni kujionea maendeleo ya ujenzi wa hizi nyumba za walimu ili tupate Majawabu,na tumekubaliana huu mradi wa hizi nyumba kufikia Septemba 18 walimu muwe mmeingia ndani kukiwa na Umeme wa Jua, Dishi la TV na TV, na tukitoka hapa leo tunakwenda kuzungumza na RUWASA aje mtu wa Maji aangalie uwezekano wa kuweka kisima kifupi kwakuwa huwezi kuweka 'tiles' na vyoo vya ndani kukiwa hakuna maji, na tunajua ili muweze kufanya kazi na hawa watoto wetu lazima muwe kwenye mazingira rafiki " Amesema Mkurugenzi.
Kwa upande wao Walimu wa Shule hiyo wamemshukuru Mkurugenzi na timu yake kwa kufika na kufanyia kikao shuleni hapo kwani imewapa morali kubwa ya kujituma katika ufundishaji.
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa