Uongozi wa Hospitali ya Mji wa Kahama na Ofisi ya Ustawi wa Jamii inamuenzi Baba wa Taifa kwa kutoa huduma ya vipimo bure kwa wazee. Huduma hii ni ya siku mbili kuanzia leo na kumalizika kesho Oktoba 14. Akifungua huduma hiyo Mgeni Rasmi Ndg. Timothy Ndanya Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama ameimwagia sifa Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa kuweza kuienzi hii siku kwa kuonesha upendo kwa Wazee. Aidha amewahakikishia Wazee waliojitokeza kupima afya zao kuwa Serikali inaendelea kuwaboreshea huduma za afya kwani Wazee ni tunu.
"Niwaombe watumishi wa afya kufanya kazi kwa Weledi, na niwaombe wazee wangu ikitokea umepewa lugha ya kejeli au kunyanyaswa na mtoa huduma wa afya Ofisi yangu ipo wazi, tuwasiliane ili tuweze kuchukua hatua stahiki". Amesema Ndanya.
Katika hatua nyingine Bw. Ndanya amewaomba wazee kuwa walimu kwenye Malezi ya Vijana na ameahidi kusimamia Sera ya wazee itekelezwe.
Awali akiongea katika utangulizi Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Halmashauri ya Mji wa Kahama Ndg. Wilfred Biragu ameiomba Serikali kutekeleza yale yaliyoahidiwa kwenye Maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Tarehe 1 Oktoba 2018.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la wazee Mji wa Kahama Ndg. Anderson Lyimo ameishukuru Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa kuweza kuwajali kwa kuwapa nafasi ya kupima afya zao ambapo itawasiadia kujua hali walizo nazo na namna ya kujiweka sawa.
Afisa Ustawi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Ndg. Abraham Kibakaya amesema kuwa wanaendelea kuwahudumia wazee kwa namna ya kipekee na tayari katika ofisi yake kuna dawati la kusikiliza kero za wazee. Amesema kuwa kwa Halmashauri ya Mji wa Kahama jumla ya wazee 6,347 wamepewa Kadi za Bima ya Afya .
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa