Waziri wa Nishati Mhe. Medard Kalemani asema Mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga utaleta fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuwa unapita Wilayani Kahama. Amesema hayo mapema leo katika Mkutano wake na wadau wa Mkoa wa Shinyanga walipokuwa wakijadili fursa zitakazo patikana kwa Bomba hilo kupita Wilayani Kahama. Katika Mkutano huo Mhe. Kalemani amewataka viongozi kuwa mabalozi wazuri katika kuwafikishia uelewa wananchi ili wasiwe vikwazo pindi utekelezaji utakapoanza.
Mhe. Kalemani amesema kuwa zaidi ya watu elfu moja wanatarajiwa kupata ajira katika ujenzi wa mradi huo, na amebainisha kuwa kipaumbele kitakuwa kwa wenyeji ambapo bomba litapita.
"Wananchi ni lazima washirikishwe na watashirikishwa kwa kiasi kikubwa sana, na hata katika kutangaza nafasi za kazi tumewalazimisha wakandarasi wale ambao wamepewa kazi kutangaza nafasi hizo za kazi kwa Lugha ya kiingereza na Kiswahili ili kuwafanya watanzania kuelewa masharti ya mikataba ile.." Amesema Mhe. Kalemani
Katika mkutano huu Mhe. Kalemani ameambatana na Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi ambaye kwa nafasi yake amewahakikishia wananchi ambao bomba litapita katika maeneo yao kuwa itafanyika tathmini na pale itakapohitajika fidia Serikali haitasita kuilipa.
Wengine walioambatana na Mhe. Kalemani ni pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati Mhe. Subira Mgalu, Katibu Wa Wizara ya Nishati na wataalamu wengine wa Wizara ya Nishati.
Ujenzi wa bomba hili unatarajiwa kuanza Mwezi wa tano mwaka huu na unatarajiwa kuisha na kuanza kazi baada ya miaka mitatu (2020).
Barabara ya Boma, Kahama
Anuani ya Posta: P.O.Box 472
Simu: +255 282710032
Simu: +255719679464
Barua pepe: md@kahamamc.go.tz / info@kahamamc.go.tz
Hakimiliki©2017. Halmashauri ya Manispaa Kahama. Haki zote zimehifadhiwa